Sikilizeni jama
Amezaliwa mwana
Mwingi wa hekima
Hana njama
Hekima bin maarifa!
Akitoka huacha mwanya
Ni kama hasi bila chanya
Buku tena sio panya
Wasemao hujidanganya
Hekima bin maarifa!
Ayajua mapana
Ya maisha tena sana
Utasema hana mana
Akeshe alale mchana
Hekima bin maarifa!
Maneno yake ingali
Tiba ya moyo halali
Ana ujazo wa akili
Pomoni, zatiririka tiritiri
Hekima bin maarifa!
Tanga yake lafudhi
Haja zote yazikidhi
Ayajua baadhi
Majukumu ya kadhi
Hekima bin maarifa!
Kimo chake cha mnazi
Paani afika pasi ngazi
Hana kiburi cha mkwezi
Wala karaha za mapenzi
Hekima bin maarifa!
Rangi yake ya eboni
Nyeusi giza totoroni
Chezo zake za utotoni
Za hadhira na fanani
Hekima bin maarifa!
Sifa zake kasi zaenea
Uwandani kama kimelea
Milele atajitanua
Miaka kwa kuendelea
Hekima bin maarifa!
©kimjisena
K