Mola wangu ewe Mola, sikia changu kilio
Mehangaikia dola,sijapata wangu mlo
Mepoteza motorola, siwezi kusema halo
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
Niliyemwita kipenzi, hivi sasa ni shubiri
Ameenda kwenye enzi, ya wampao sukari
Kisa hatuli viazi, kaenda bila habari
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
Mimi changu kibarua, kuokota takataka
Nayajaza magunia, pomoni bila mipaka
Ndipo nitapata mia, ama nipewe nafaka
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
Ndugu zangu majirani, wanitenga ka ukoma
Wa bara hadi pwani, wanisema kwenye ngoma
Mimi niko taabani, angalau ningesoma
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
Wanibeza watoto, kwa kuniita tahira
Wamekuwa kama moto, lini tapata ajira
Maisha kama kokoto, ndio wangu ujira
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
Narudi kwako Rabana, wewe mtoa riziki
Sitaki mi kujifanya, kama wenye pikipiki
Nisamehe ewe Bwana, niepushe na mikiki
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.
©kithi21
K